Shirika la Nyumba nchini litaanza ujenzi wa ofisi zake katika kaunti ya Kisii kwanzia mwezi ujao, haya ni kwa mjibu wa kaimu waziri wa Ardhi na Nyumba ambaye pia ni waziri wa Teknolojia na Mawasiliano nchini Fred Matiang'i.
Matiang'I, akiongea siku ya Jumamosi katika mji wa Kisii, alisema kuwa uwekaji wa msingi wa makao hayo utaanza chini ya mwezi mmoja ujao, na akadokeza kuwa tayari kwa ushirikiano wa gavana wa Kisii eneo la ujenzi huo lishaa tambuliwa.
Waziri huyo alifafanua kuwa hii ni harakati mojawapo wa kuhakikisha kuna makao ya kutosheleza wakazi wa Kisii, na pia akaongeza kusema kwamba ni juhudi za serikali ya Jubilee kuona kuwa kila kaunti nchini inafaidi kutokana na mradi wa serikali wa kuboresha makazi na mazingira ya kuridhisha.
“Serikali yetu imejitahidi kuona kwa kila mwananchi ananufaika na ana makao mazuri pamoja uimarishaji wa mazingira yenye hewa safi na ya kupendeza,” alisema Bwana Waziri.
Matiang'i pia alidokeza kuwa mradi wa kuweka nyaya za kusambaza mtandao wenye kasi wa awamu ya pili utaanza, ili kuhakikisha kuwa kaunti yote ya Kisii na ofisi zote zimeunganishwa kabla ya mwisho wa robo ya mwaka huu ili kuwezesha upatikanaji wa habari kwa haraka.
Awamu ya kwanza ya mradi huo kwenye kaunti hiyo ulifika katika makao makao makuu ya ofisi za bunge la kaunti na ile ya Gavana wa Kisii.