Kituo cha kurekebisha tabia cha Reachout chenye makao yake mjini Mombasa kimeanzisha zoezi la kutoa mafunzo yanayonuia kulinda haki za waraibu wa mihadarati pamoja na makahaba.
Akizungumza siku ya Jumanne kwenye mkutano ulioleta pamoja mashirika mbalimbali yasiyo ya serikali, afisa msimamizi wa Reachout, Taib Abdulrahaman, alisema kuwa wanalenga kutumia mafunzo hayo kutoa hamasa kwa jamii, kuhusu namna ya kutangamana na watu kama hao pasi na kuwanyima haki zao za kikatiba.
“Kama jamii lazima tufahamu kuwa watu hawa pia wanahaki kama wengine, hivyo sharti tuziheshimu haki zao na tutangamane nao bila kuwabagua,” alisema Taib.
Afisa huyo vilevile alieeleza imani yake kuwa kupitia zoezi hilo jamii itapata kuelimika na kutokomeza unyapapaa dhidi ya watu wanaotumia mihadarati pamoja na makahaba.
“Katiba inaeleza wazi kuwa kila mtu ana haki kupata huduma muhimu, hivyo hatufai kubagua mtu kwa msingi wa uraibu wake,” alisema Taib.
Kituo cha Reachout husadia waraibu wa mihadarati kurejelea hali yao ya kawaida kwa kuwapa ushahuri nasaha na pia kuwapa dawa zinazosaidia kupunguza makali ya baadhi ya dawa wanazotumia.