Shirika moja ambalo limekuwa likitoa mitihani ya miigo kwa shule mbalimbali za msingi katika Kaunti ya Nyamira limeshtumiwa na baadhi ya walimu kutoka eneo hilo.
Samuel Nyangena, mwenyekiti wa bodi ya usimamizi wa mitihani ya shule za msingi Nyamira, aliwaomba wanachama wake kususia mitihani hiyo hadi pale makubaliano ya utendakazi na ushirikiano yataafikiwa kati ya bodi hiyo na washirikishi wa mitihani hiyo.
"Tungependa kuwaomba walimu wote kutoka shule zote za msingi Nyamira kususia mitihani hiyo hadi pale mstakabali wa utendakazi utakapo afikiwa baina yetu na shirika hilo la mitihani," alisema Nyangena.
Kulingana na Nyangena, mitihani hiyo ilikuwa akiwatia hofu wanafunzi kwa kuwa maswali yaliyomo kwenye karatasi hizo hayamo kwenye mtaala wa silabasi mpya.
"Kama bodi tumeangalia mitihani hiyo nakubaini kuwa ilikuwa ikiwatia hofu watahiniwa kwa kuwa maswali yaliyomo hayamo kwenye mtaala wa silabasi mpya. Hiyo ndiyo sababu tumeamua sharti kuwepo mstakabali wa utendakazi baina ya shirika hilo na sisi,” alisema Nyangena.
Kwa upande wake, afisa mshirikishi wa shirika hilo la Dr Joy Kerubo Foundation, Kefa Osoro, alisema kuwa yuko tayari kukutana na walimu hao ili kujadili swala hilo ila akasisitiza kuwa nia ya shirika hilo nikuinua viwango vya elimu miongoni mwa wanafunzi.
"Sipingi pendekezo la kukutana na walimu ili kujadili swala hili ila isije ikawa njia yakuathiri shughuli zakuinua viwango vya elimu katika eneo hili,” alisema Osoro.