Shirika moja lisilo la kiserikali limeanzisha mpango wa kuwahamasisha wanawake mjini Mombasa, kuhusu athari za itikadi kali.
Shirika la Coast Education Center linatumia magari ya usafiri maarufu kama matatu, kuwakutanisha wanawake hao kwa kuwalipia nauli katika vituo mbalimbali vya kuabiri magari, ambapo pia wanapata fursa ya kuzungumza nao.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumamosi, mkurugenzi wa shirika hilo Bi Halima Mohamed alisema mbinu hiyo inawasaidia kulenga wanawake wengi mjini humo hasa wakati wa asubuhi na jioni.
“Tunalenga wanawake wanaoenda kazini na hata wasiofanya kazi. Tunawaelimisha kuhusu zile dalili ndogo ndogo zinazoweza kuwashawishi kujiingiza katika itikadi kali,” alisema Bi Halima.
Halima, aliongeza kuwa wanawake hasa Mjini Mombasa wanafaa kujihusisha zaidi na kazi zinazoweza kukuza na kuimarisha familia zao, badala ya kujiingiza katika mafunzo yanayowapotosha.
Katika mpango huo uliopewa jina la “Mini Bus”, gari aina ya matatu iliyowekwa kibandiko maalum huegeshwa katika kituo cha kuabiri magari, ambapo wanawake husafirishwa katika maeneo wanayokwenda, huku wakipewa mafunzo hayo na wataalam.
Baadhi ya vituo lengwa ni Likoni feri hadi Bamburi, Kiembeni miongoni mwa maeneo mengine.
Halima alisema kwamba hiyo ni moja tu kati ya miradi mingi wanayopania kuanzisha ili kusaidia akina mama mjini humo.