Bodi za shule zote katika kaunti ya Kisii zimeshauriwa kuwa na ushirikiano mwema na walimu wakuu ili kufanikisha viwango vya elimu kuinuka zaidi katika kaunti hiyo.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa viwango vya elimu hudorora katika mashule kufuatia ukosefu wa ushirikiano mwema kati ya walimu wakuu wa shule na bodi za shule.
Akizungumza siku ya Jumatatu afisini mwake, mwenyekiti wa bodi ya elimu katika kaunti ya Kisii Henry Onderi aliomba kila bodi ya shule kushirikiana na usimamizi wa shule ili viwango vya masomo kuinuka katika kaunti ya Kisii.
“Kudorora kwa elimu huchangiwa na kutoshirikiana kati ya walimu wakuu wa shule na bodi za shule, naomba washirikiane ili viwango vya masomo kuinuka hapa kisii,” alisema Onderi.
Wakati huo huo, Onderi alisema yeyote atakayefumaniwa akikiuka majukumu yake atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha, aliomba washkadau wote wa elimu kuwa pamoja na kushirikiana kuhakikisha viwango vya masomo vimeinuka katika kaunti ya Kisii.