Share news tips with us here at Hivisasa

Zaidi ya wakulima 200,000 wa ng’ombe wa maziwa wamejiunga na shirikisho la kutetea maslahi ya wakulima hao kote nchini.

Hatua ya wakulima hao inalenga kuwaleta pamoja kama wafugaji wa ng’ombe wa maziwa ili kuwa na sauti moja ya kutetea maslahi yao.

Muungano huo chini ya shirikisho la wakulima husika la Kenya Dairy Farmers Federation umevutia vyama vya ushirika vya wafugaji wa ng’ombe wa maziwa 26.

Afisa mkuu wa KDFF David Bett, alielezea matumaini ya shirikisho hilo kubadilisha maisha ya wakulima hao.

Akihutubia wanahabari mjini Eldoret, Bett alisema kuwa kwa miaka mingi maslahi ya wakulima hao imekuwa ikipuuzwa kutokana na ukosefu wa shirika spesheli la kushughulikia matakwa ya wakulima katika sekta ya maziwa.

“Kwa miaka mingi wakulima wa ng’ombe wa maziwa wameachwa kama mayatima bila shirika la kutetea maslahi yao, natumai kuanzishwa kwa shirika hili kutawezesha wakulima wetu kuwa na sauti ya kuwasilisha hoja zao kwa wadau wote katika sekta,” alisema Bett

Shirikisho hilo, ambalo lilianzishwa yapata miaka mitano iliopita, tayari limeshika kasi ya kupigania maslahi ya wakulima.

Hivi maajuzi, maafisa wakuu wa shirika hilo walionya kwamba hawatavumilia tabia ya wamiliki wa viwanda vya kutengeneza na kuifadhi maziwa ya kushukisha bei ya kununua maziwa bila kuhusisha wadau wote.

Tayari shirikisho hilo limetishia kuongoza wakulima kususia kuwasilisha maziwa yao kwa viwanda husika iwapo viwanda hivyo vitaendelea na tabia hiyo.