Shughuli za kawaida jijini Mombasa zimetatizwa kwa muda kufuatia maandamano ya wafuasi wa Cord.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wamiliki wengi wa biashara walifunga biashara zao kwa kuhofia mali yao kuporwa na kuharibiwa.

Polisi walitumia vitoa machozi kuwatawanya wafuasi hao waliokuwa wakiandamana kushinikiza kubanduliwa kwa makamishna wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC.

Ilimlazimu Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho kuwatuliza wafuasi hao ili kuzuia makabiliano kati yao na polisi.

"Tunawaomba wakaazi jamani tuwe na subra na tufanye maandamano yetu kwa njia ya amani hadi pale IEBC itakapovunjwa,” alisema Joho siku ya Jumatatu.

Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir kwa upande wake aliwataka maafisa hao kusitisha makabiliano hayo kwa kusema kuwa maandamano hayo yalikuwa ya amani.

Aidha, aliwaonya viongozi dhidi ya kuwachochea wafuasi hao ili kuzua rabsha.

"Tumekuja kufanya maandamano ya amani bila fujo lakini tafadhalini viongozi msiwahadae vijana wetu wafanye fujo na kusababisha harasa. Tuwe makini na tufanye maandamano kwa haki,” alisema Nassir.

Mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba alisema kuwa maandamano hayo ni ya kikatiba na lazima Tume ya IEBC kung’atuka mamlakani, huku akiwataka maafisa wa polisi pamoja na wafuasi wao kudumisha amani ili kuzuia kushuhudiwa machafuko.

Watu wasaba walitiwa mbaroni wakati wa maandamano hayo ikiwemo Spika wa Bunge la kaunti ya Mombasa Thadius Rwajay, Mwakilishi wa Wadi ya Junda Paul Onje na wafuasi wengine wa mrengo huo wa Cord.