Shughuli za masomo zilirejelewa katika shule za umma kote nchini mapema leo, kufuatia kufutiliwa mbali kwa mgomo wa kitaifa wa walimu uliokuwa umedumu kwa takribani majuma mawili.

Share news tips with us here at Hivisasa

Jijini Kisumu, shughuli za masomo ziling’oa nanga na kuendelea mbele kwa njia shwari, baada ya walimu na wanafunzi kufika shuleni mapema Jumatatu.

Mwandishi huyu alitembelea shule mbali mbalij jijini Kisumu miongoni mwao shule ya msingi ya Arya, shule ya msingi ya Lake na shule ya upili ya wasichana ya Kisumu, ambapo masomo yalikuwa yakiendelea.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Arya Mark Ochieng, alisema kuwa walimu wamezama kazini kwa bidii, hasa baada ya kuwa nje ya madarasa kwa takribani miezi miwili.

“Katika gwaride tulikuwa na wanafunzi wote pamoja na walimu, na kulikuwa na ishara kwamba wanafunzi walikuwa na hamu sana ya kurudi shuleni,” akasema mwalimu huyo mkuu.

Baadhi ya wanafunzi tuliozugumza nao, walisema kuwa wako tayari kutia bidii masomoni, baada ya kupoteza majuma mawili kutokana na mgomo wa kitaifa wa walimu.

Naye Mkuu wa elimu Wilayani Kisumu Mashariki Jane Mutange, alisema kuwa shule zote katika eneo hilo zilifunguliwa mapema Jumatatu, na masomo yanaendelea kama ilivyopangwa.

Juma lililopita, mahakama ya viwanda jijini Nairobi iliwaagiza walimu kufutilia mbali mgomo wao wa kitaifa, uliokuwa umelemaza shughuli za masomo kwenye shule za umma kote nchini kwa takribani majuma mawili.