Chama cha kutetea maslahi ya walimu nchini KNUT kimetoa makataa ya mwezi mmoja kwa usimamizi wa shule za Bridge International kufunga mabewa ya shule hiyo katika eneo la Gusii.
Kwenye kikao na wanahabari mjini Kisii siku ya Jumatano, mwekahazina wa chama hicho John Matiang'i alishtumu shughuli za shule hiyo huku akisema usimamizi wa shule hiyo haufuatilii mtaala wa elimu nchini.
"Inakuaje kwamba shule ya Bridge International inatoa mafunzo yaliyo nje ya mtaala wa elimu nchini na hata hatuelewi na ni kwa sababu gani wanadai kuwa utoaji huduma za elimu ni nafuu ilhali wanalipisha karo za juu," alishangazwa Matiang'i.
Matiang'i aidha alisema iwapo matawi ya shule hiyo hayatofungwa kwa kipindi cha mwezi mmoja itawalazimu walimu kuandamana kusinikisha kufungwa kwake kwani anadai shughuli za shule hizo ni za kibiashara na wala sio kwa kutoa huduma za elimu nchini.
"Ikiwa kwamba matawi ya Bridge International katika eneo la Gusii hayatofungwa kwa mwezi mmoja ujao, basi itawalazimu walimu kuandamana ili kusinikisha kufungwa kwa matawi hayo," aliongezea Matiang'i.