Mbunge wa Mugirango magharibi James Gesami ameombwa kusaidia shule ya msingi ya Ekenyoro kujenga vyoo vipya vya wanafunzi wasichana wa shule hiyo.
Akiongea siku ya Jumatano katika shule hiyo ya Ekenyoro, mwalimu mkuu wa shule hiyo Peter Ombogo aliomba msaada huo baada ya vyoo vya wasichana wa shule hiyo kuanguka kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika eneo la Kisii.
Ombogo alisema vyoo hivyo vilikuwa vinatumika na wanafunzi 300 ambao ni wasichana na kulazimika sasa kutumia vyoo vya wavulana na kusababisha msongamamo mkubwa.
“Vyoo vya wasichana vilianguka na shule yangu ina wanafunzi zaidi ya 600 ambao sasa wanatumia vyoo vya wavulana, ninaomba mbunge wetu Gesami kupitia hazina ya ustawi maeneo bunge CDF kutusaidia kujenga vyoo vipya,” alikiri Ombogo.
Mwalimu huyo pia aliomba wahisani wema kujitokeza kushirikiana kutoa usaidizi kwa ujenzi huo wa vyoo vipya kwani sasa mazingira katika shule hiyo sio ya kufaa kwa wanafunzi.