Shule ya Msingi ya Nyangiti iliyoko wadi ya Kegogi Kaunti ya Kisii imefungwa hadi wakati usiojulikana.
Wakizunguza na waandishi wa habari mnamo siku ya Jumanne katika shule hiyo ya Nyangiti, wazazi wa shule hiyo waliamua kuifunga shule hiyo na wanafunzi kuenda nyumbani hadi wakati usiojulikana kufuatia walimu watatu kuhamishwa kuenda shule zingine mwalimu mkuu wa shule hiyo akiwa mmoja wao.
Jambo hilo halikuwafurahisha wazazi hao na kutaka walimu hao warudishwe la sivyo shule hiyo ibaki imefungwa
“Tumeifunga shule hii maana tunahitaji walimu waliohamishwa warudishwe. Hatutaki wengine tofauti,”alisema Cornellius Mireri, mzazi wa shule hiyo.
Wiki tatu zimepita tangu shule zifunguliwe kote nchini jambo ambalo limewapelekea watu wengi wa eneo hilo kushangazwa na kwa kufungwa kwa shule hiyo kabla ya wanafunzi kupata elimu.
Afisa wa elimu katika zone ya Ng’enyi Shem Ogugu, kupitia simu alisema kua hajui chochote kinachoendelea katika shule hiyo na kukana kuwa hajawai pokezwa malalamishi yoyote kutoka kwa wazazi hao.
Wazazi kwa upande wao wanadai kuwa walimwalika kuja shuleni humo na hakufika na kuamua kuifunga shule hiyo.
Aidha afisa huyo aliahidi kufuatilia mambo hayo ili kuafikia suluhu haraka ili wanafunzi waweze kuendelea na masomo yao kama kawaida.
“Nitahakikisha kuwa jambo hilo la kufungwa kwa shule na walimu kuhamishwa litaangaliwa hivi karibuni,”alisema Ogugu.