Usimamazi wa shule ya msingi ya Riooga ukiongozwa na mwalimu mkuu wa shule hiyo umewaomba wahisani kujitokeza na kuwasaidia kuziba nyufa na kurekebisha paa za shule hiyo ambazo zimekuwa kero kwa mda sasa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kulingana na mwalimu mkuu, Joshphat Ratemo, wanalizimika kuwaruhusu wanafunzi kwenda nyumbani mapema ili kujisitiri wakati wa mvua. 

"Usimamizi wa shule hii hulazimika kuwaruhusu wanafunzi kwenda nyumbani kila mchana, hasa kwenye msimu huu wa mvua ili kujisitiri kutokana na mvua kwa kuwa paa za shule hii zina nyufa, hali inayofaa kurekebishwa," alisema Ratemo.

Ratemo vilevile aliongeza kwa kusema kuwa shule hiyo haijapokea pesa zozote kutoka kwa hazina ya pesa za maendeleo ya eneo bunge la Kitutu Masaba, hata baada ya afisi ya CDF eneo hilo kuwaahaidi kuwatengea shillingi nusu milioni.

"Kwa sasa tuko katika hali mbaya sana na tungependa kuomba msaada wa dhararu hasa kutoka kwa viongozi wa eneo hili, na kufikia sasa tunashangazwa mbona afisi ya maendeleo ya eneo bunge hili la Kitutu Masaba haija harakisha kutupa hundi ya nusu milioni tuliyoahidiwa na mbunge wa eneo hili Timothy Bosire," aliongezea Ratemo.

Kulingana naye, wanafunzi wamekosa kumaliza silabasi kwa kuwa walikuwa nyumbani kwa mwezi mmoja walimu walipokuwa kwenye mgomo, na sasa imewawia vigumu hata kuwaandaa wanafunzi wa darasa la nane wanaotarajiwa kuanza mitihani yao mapema mwezi ujao. 

"Ni chini ya mwezi mmoja tangu tufungue shule kwa muhula wa tatu, na huenda ikawa vigumu kumaliza silabasi kwa kuwa wanafunzi hawapati wakati mzuri kusomeshwa kutoka na mvua inayoendelea kunyesha, swala ambalo tumeliwasilisha kwa wizara ya elimu lakini hadi sasa hamna hatua iliyochukuliwa," aliongezea. 

Mwalimu huyo mkuu aidha ameiomba serikali ya kaunti kuingilia kati na kusaidia kwenye hali hiyo kwa kuwa sasa wanafunzi wa shule hiyo hasa wa darasa la nane wanaendelea kuumia hata zaidi. 

"Nafikiri serikali ya kaunti hii ilikuwa imetenga kiasi fulani cha pesa za kupambana na mvua ya El-nino na ningeomba serikali ya kaunti ya Nyamira ichukulie swala hili kama la dharura na kutusaidia na pesa kidogo zilizotengewe El-nino ili kurekebisha hali," alimalizia kusema.