Wanafunzi na walimu wa shule za msingi kutoka eneo bunge la Borabu wana kila sababu ya kutabasamu baada ya mwanasiasa wa eneo hilo kuhaidi kuwanunulia tarakilishi na mashine za kuchapisha mitihani ili kuwapunguzia matumizi ya fedha. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubu kwenye shule ya msingi ya Riosando siku ya Jumatatu, mwanasiasa huyo, Nyandoro Kambi alisema kuwa wakfu wake wa Nyandoro Foundation tayari umetenga shillingi millioni tano, pesa zitakazonunua tarakilishi hizo pamoja na mashine za kuchapisha mitihani itakayosambazwa kote Borabu.

Aliongeza kusema kuwa mashine hizo zitakuwa katika shule zote za eneo hilo kuanzia Januari mwaka ujao, na akawasihi walimu kuchangamkia swala hilo ili kusaidia kuinua viwango vya elimu katika eneo hilo. 

"Tayari wakfu wangu umetenga shillingi millioni tano, pesa zitakazonunua tarakilishi na mashine za kuchapisha mitihani, mashine ambazo zitasambazwa katika shule zote za msingi huku Borabu, na ninawahaidi kuwa kufikia januari zitakuwa zimefika," alisema Nyandoro. 

Mwanasiasa huyo aliongeza kwa kusema kuwa atawaajiri mafundi watakao kuwa wakiziangalia tarakilishi hizo mara kwa mara, na akawahimiza wazazi kushirikiana na shule zao ili kusaidia kuimarisha elimu miongoni mwa watoto wao.

"Mafundi ambao ni wataalam wa tarakilishi watakaoajiriwa watalipwa na wakfu wangu, na ningependa kuwahimiza wazazi washirikiane na shule wanakosomea wanao ili kuwapa motisha walimu kuwapa wanao mafunzo yanayofaa," aliongezea Nyandoro.