Shule zote za upili zilizoko katika eneo bunge la Nyaribari Masaba zimeahidiwa kupewa basi iwapo zitaboresha matokeo yao katika mitihani ya kitaifa.
Hii ni mojawapo ya harakati za kuhakikisha kuwa viwango vya elimu katika eneo bunge hilo, vimeboreshwa na kuimarishwa zaidi hasa katika shule zote za sekondari.
Akizungumza siku ya Ijumaa katika shule ya upili ya St Charles Lwanga Ichuni, kwenye hafla ya kupokeza rasmi basi la shule kwenye usimamizi wa wa shule hiyo, mbunge wa eneo hilo Elijah Moindi aliwataka walimu, wazazi pamoja na wanafunzi kutia bidii na kushirikiana ili kuinua viwango vya elimu kwenye eneo bunge hilo.
Mbunge huyo aliwasifu walimu wa shule hiyo pamoja na wanafunzi wa mwaka jana kwa kufanya vizuri katika mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne
“Ningependa shule zote zifuate mkondo wa shule hii kwa kufanya vizuri katika mtihani wa kitaifa. Nitazawadi shule itakayo fanya vyema katika mtihani kwa kuinunulia basi, alisema Moindi.
Mbunge huyo ameanza ziara ya kuzitembelea shule zote za msingi na za upili katika eneo hilo ili kukagua miradi inayofadhiliwa chini ya pesa za hazina ya maendeleo ya maneneo bunge.