Mamlaka ya usafiri na usalama wa barabarani NTSA sasa imeshtumiwa kwa kile kinachotajwa kama hatua yake ya kujaribu kulemaza shule zinazotoa mafunzo ya uendeshaji wa magari.
Ni shutma ambazo zimetolewa na muungano wa kitaifa wa shule zinazotoa mafunzo ya uendeshaji wa magari wa The Kenya National Driving School Association- KNDSA ukiongozwa na mwenyekiti wake John Mwatha.
Muungano huo sasa umetishia kushtaki mamlaka hiyo kwa kukosa kujadiliana nao kabla ya kubuni mtaala ( curriculum) mpya unaofaa kutumiwa katika shule hizo zinazotoa mafunzo hayo ya uendeshaji wa magari.
Mwatha amelalama kwamba muungano huo umewekeza pakubwa katika sekta hiyo huku akidai kwamba baadhi ya yaliyopendekezwa kwenye mtaala huo mpya hayawezi kuafikiwa.
Amehoji kwamba maswala kama vile la kutokuwa na magari kwa zaidi ya miaka minane na lile la kuwa na kipande cha ardhi kisichokuwa chini ya ekari 6 ili kupewa leseni ya kuendeleza shule inayotoa mafunzo ya uendeshaji wa magari hayafai.
Mwatha anakariri kuwa tangu muungano huo ulipobuniwa mwaka wa 1987, shule zinazotoa mafunzo ya uendeshaji wa magari zimekuwa zikiwapa mafunzo kwa waendeshaji magari kwa kutumia magari mbalimbali huku mengine yao yasiyokuwa mapya na leseni za uendeshaji magari zimekuwa zikitolewa kwa wale ambao wamekuwa wakipita mitihani ya uendeshaji wa magari.
Amehoji kwamba huenda kuna nia fiche kuhusiana na hatua ya mamlaka ya NTSA ya kutaka mtaala huo mpya utumike ilhali maswala mengi yaliyo kwenye mtaala huo yametolewa kwa mtaala wa uendeshaji wa magari kutoka nchini Uswizi (Sweden).