Share news tips with us here at Hivisasa

Idara ya Elimu katika Kaunti ya Mombasa imetoa onyo kwa shule zitakazopatikana zikiendeleza masomo ya ziada wakati huu wa likizo.

Hii ni baada ya madai kutokea kwamba baadhi ya shule bado zinaendeleza masomo hayo licha ya serikali kupiga marufuku.

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumamosi mjini humo, mkurugenzi mkuu wa elimu Kaunti ya Mombasa Abdulkadir Kike alisema kuwa wanashirikiana na wadau wa elimu kuhakikisha kuwa shule zinazokiuka agizo hilo zinachukuliwa hatua.

“Tukipata ripoti yoyote tutachukua hatua ili kuona kwamba jambo hilo linakomeshwa kwa sababu masomo ya ziada yalikatazwa kabisa,” alisema Kike.

Mkurugenzi huyo aidha alisema bado hawajapokea ripoti yoyote kuhusiana na swala hilo kufikia sasa, lakini wanafuatilia kwa makini kujua iwapo kuna madai yoyote yatakayojitokeza.

Hata hivyo, wakaazi waliozungumza na mwandishi huyu mjini humo walisema baadhi ya shule zinatumia ujanja ambapo wanafunzi wanahudhuria masomo hayo wakiwa wamevaa nguo za nyumbani ili kuzuia kutambuliwa.

“Wanafunzi huwa wanavaa nguo za nyumbani wanpoenda shuleni wakati wa likozi. Wakitembea barabarani ni vigumu kujua kuwa wanaenda shuleni,” alisema mkaazi mmoja.

Mwaka jana, Wizara ya Elimu nchini ilitoa agizo kwa shule zote kusitisha masomo ya ziada kwa wanafunzi wakati wa likizo.

Agizo hilo lililenga kuwapa wanafunzi muda wa kupumzika na kutangamana na familia kabla shule kufunguliwa kwa muhula unaofuata.

Agizo hilo pia lilitolewa kutokana na madai kwamba shule hizo zimekuwa zikiwatoza wazazi fedha za ziada kugharamia masomo hayo.