Waziri wa Utalii Najib Balala amesema kuwa nia yake kwa sasa ni kuwatumikia wananchi wa Kenya kwa wadhifa wa uwaziri na si kuzungumzia siasa za ni nani atamridhi Hassan Joho kama Gavana wa kaunti ya Mombasa.
Wandani wa Balala Ibrahim Khamis pamoja na Ben Furaha wanasema kuwa waziri amekuwa akijihusisha na maswala ya uwaziri na kuwa hataki kujihusisha sana na siasa.
“Hajatamka lolote kwangu wala kuzungumzia mada hiyo,” alisema Khamis.
Furaha ambaye kwa wakati mmoja alikuwa msaidizi wa waziri Balala alisema kuwa waziri amekomaa kisiasa na anajua wakati mwafaka wa kuzungumzia siasa.
Baadhi ya wakaazi wa mji wa Mombasa wamekuwa wakimlaumu Gavana Joho kwa kutofanya vya kutosha kuhakikisha kuwa mji wa Mombasa unakuwa msafi.
Pale awali mji wa Mombasa uliorodheshwa kama mji msafi nchini wakati Najib Balala alikuwa meya wa mji huo.
Siku ya Ijumaa Balala alisema kuwa atakuja na mipango yake baadaye huku wengi wakisema kuwa huenda ana nia ya kuwania ugavana katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.
“Tutajenga nchi hadi mwaka wa 2021. Hatutazungumzia siasa za mwaka wa 2022. Hatuwezi kuwa tunapiga siasa wakati wote. Misimamo hii haina umuhimu wowote iwapo hakutakuwa na maendeleo nchini,” alisema Balala.
Kufikia sasa, wanasiasa kadhaa wameonyesha nia ya kumridhi Joho.
Wanasiasa hao ni Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo, mwenzake wa Mvita Abdulswamad Nassir pamoja na aliyekuwa mbunge wa Nyali Cyprian Awiti.
Aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar pia ameonyesha nia ya kumridhi Joho kama gavana wa Mombasa.