Afisa wa Maswala ya Kijinsia na Haki za Watoto katika Shirika la Haki Afrika amesema kuwa huenda siasa za chuki, uchochezi na mabishano zinazoendelezwa humu nchini zikasababisha mgawanyiko mkubwa pindi uchaguzi mkuu ujao utakapowadia na kudidimiza uchumi wa taifa.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza katika afisi za Shirika hilo mjini Mombasa siku ya Jumatano, Salma Hemed alisema kwamba malumbano hayo miongoni mwa wanasiasa tayari yamewagawanya baadhi ya Wakenya katika misingi ya kisiasa mashinani.

Kulingana na Hemed, iwapo tume ya uiano na utangamano wa kitaifa NCIC italegeza msimamo wake, basi huenda wanasiasa hao wakahatarisha mshikamano wa taifa hili katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

"Tumeona kuwa siasa za chuki, uchochezi na malumbana ya kisiasa huenda yakavurugu usalama wa taifa hili na kusababisha hasara kubwa ikiwemo kudidimia kwa uchumi. Wakanya wengi huenda wakalumbana iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa kuzuia siasa kama hizo,” alisema Hemed.

Aidha, aliwasihi wanawake kujitokeza na kuendeleza kampeni za amani mashinani ili kuwakinga vijana kutokana na maswala ya uhalifu hasa wakati huu ambapo kampeni za uchaguzi wa mwaka wa 2017 zinazidi kupamba moto.