Siasa za kiti cha ubunge wa kisauni zinaendelea kupamba moto huku mbunge wa eneo hilo Rashid Bedzimba akisisitiza kuwa hakuna mtu yoyote atakayepata tiketi ya moja kwa moja kupitia chama cha ODM.
Akizungumza nje ya afisi yake baada ya kutoa msaada wa vyakula vilivyogharimu shilingi milioni moja, Bedzimba alisema kuwa chama cha ODM ni chenye demokrasia iliyowazi hivyo iwapo yeyote ana nia ya kutumia chama hicho basi ajitayarishe kupitia kwa mchujo utakaoamuliwa na wananchi na sio kinara yoyote wa chama.
“Nataka kuwaambia yeyote anayepanga kutumia tiketi ya ODM kwamba hakuna nafasi ya moja kwa moja bali ajiandae kwa mchujo,” alisema mbunge huyo.
Kauli yake hii inajiri baada ya mpinzani wake wa karibu Ali Mbogo kusema kuwa tayari ameahidiwa tiketi ya moja kwa moja na kinara wa chama hicho Raila Odinga wakati walipokuwa kwenye safari za kibiashara nchini Ujerumani huku Bedzimba akisema kuwa ameelewana na Raila kuwa mchujo ndio uamue atakayepeperusha bendera ya chama cha ODM kwenye ubunge wa eneo hilo la Kisauni.
Wakati huo huo Bedzimba amewataka wakaazi wa maeneo ya kisauni na viunga vyake kudumisha usalama huku taifa likielekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka ujao na kuwahimiza vijana kutokubali kutumiwa vibaya na mwanasiasa yoyote ili kuhujumu amani ya wakenya wenzao.