Joto la kisiasa baina ya mirengo ya Jubilee na Cord linalozidi kupamba moto nchini kwa sasa tayari limeanza kuwatia hofu wafanyibiashara wa hoteli katika eneo la Pwani.
Kwenye mahojiano na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Jumatano, mwenyekiti wa Muungano wa Wahudumu wa Hoteli Pwani, Sam Ikwaye, alizitaja siasa hizo kama zinazohatarisha sekta ya utalii.
Kulingana na Ikwaye, ikiwa hali hiyo itaendelea hadi taifa litakapoandaa uchaguzi mkuu mwaka ujao, huenda wenye hoteli wakakadiria hasara kubwa kwani watalii wengi wa kigeni wataogopa kuzuru nchini kutokana na hofu ya machafuko kama yaliyoshuhudiwa wakati wa uchaguzi wa nwaka 2007.
“Hatukatazi wanasiasa kupiga siasa kwani ni jambo la kawaida kwao. Hata hivyo, wanapaswa kusubiri wakati wa uchaguzi ufike ndio wapige hizo siasa zao. Hakuna mgeni atazuru Kenya iwapo itakuwa ni kujibizana kila siku,” alisema Ikwaye.
Afisa huyo alisema kuwa sekta ya utalii iliadhirika mwaka 2007 kufuatia vurugu za baada ya uchaguzi, jambo ambalo liliwafanya wafanyibiashara kufunga biashara zao hasa baada ya mataifa ya kigeni kuwaonya wananchi wao dhidi ya kuzuru Kenya.
Aidha, Ikwaye alifichua kuwa wamiliki wa hoteli katika ukanda wa Pwani tayari wanakadiria kushuka kwa biashara hasa kipindi hiki ambapo kunashuhudiwa idadi ndogo ya watalii wanaozuru eneo hilo.