Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto walilazimika kukatiza ziara yao katika eneo la Kitutu Masaba siku ya Jumatano.

Share news tips with us here at Hivisasa

Rais Kenyatta, ambaye hapo awali alikuwa amehudhuria hafla ya kupandishwa hadhi kwa Hospitali ya Nyamira Level Four, barabara ya Kebirigo-Mosobeti pamoja na Chuo cha anuwai cha Egetai, alitarajiwa kuzindua mradi wa maji wa Nyangori kabla ya uzinduzi huo kukatizwa.

Msafara wa rais ulikuwa tayari umefika katika mradi huo wa maji kabla ya ratiba yao kubadilishwa ghafla kufuatia ripoti za ujasusi zilizoashiria uwezekano wa kushuhudiwa kwa vurugu.

Uchunguzi wa kipekee uliofanywa na mwandishi huyu uliashiria kuwa mgombea kiti cha ugavana Walter Nyambati na mwanasiasa wa Kitutu Masaba Shadrack Mose walikuwa wamewasafirisha watu kutoka sehemu mbalimbali katika mpango wa kuwaaibisha Mbunge Timothy Bosire na mwanasiasa Charles Mochama.

"Ukweli ni kwamba tulikuwa tumenunuliwa filimbi na Nyambati na Mose ili kuvuruga hotuba za Bosire na Mochama iwapo wangepewa fursa ya kuhutubia umati. Tulikuwa tumejipanga tangu asubuhi,” alisema kijana mmoja aliyezungumza na mwandishi huyu kwa sharti la kutotajwa.

"Lengo letu lilikuwa kuwapa wawili hao wakati mgumu. Rais na naibu wake wanakaribishwa hapa kwa kuwa sisi hatuna ubaya nao,” alisema kijana huyo.

Aliongeza, "Tulitaka kuzuke uhasama baina ya Bosire, Mochama na wakaazi kwa manufaa ya waliotuajiri na hatuna majuto yoyote”.

Jitihada za kupata maoni ya wanasiasa waliotajwa viligonga mwamba baada yao kukosa kujibu simu.