Mbunge wa Nakuru Magharibi Samuel Arama ameshikila msimamo wake wa kuigura chama pinzani cha ODM na kujiunga na chama tawala cha Jubilee na kuwa hajutii lolote baada ya kuchukua hatua hiyo. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Arama ambaye ameonyesha kughadhabishwa kwake na baadhi ya wabunge wa ODM waliomzomea rais Uhuru Kenyatta akitoa hotuba yake bungeni ameeleza kuwa Jubilee imetumikia wananchi vilivyo na uleta maendeleo mengi ikilinganishwa na serikali zilizopita.

"Serikali ya Jubilee imeleta maendeleo mengi nchini ikilinganishwa na serikali zilizopita. Sikukosea hata kidogo kujitenga na ODM ambayo kazi yao ni kuzua vurugu na kukashifu serikali kila wakati. Haya ni mambo ambayo hayawezi kuleta maendeleo nchini," alielezea Arama.

Mbunge huyo ambaye alikuwa akizungumza katika eneo bunge lake siku ya Jumanne pia amewaomba wafuasi wa ODM na vyama vingine kuungana naye katika chama cha Jubilee ili kuiunganisha kaunti ya Nakuru chini ya chama kimoja.

"Ninatoa wito kwa wakaazi wote wa kaunti ya Nakuru kuungana pamoja na kuunga mkono Jubilee ili kaunti hii iwe chini ya chama kimoja kabla ya uchaguzi wa mwaka ujao. Tunalohitaji sasa ni maendeleo na haya yatawezekana sote tukiwa Jubilee," Arama aliongezea.