Huku hafla ya siku tatu ya uhamasisho dhidi ya athari za matumizi ya dawa za kulevya na unywaji wa pombe haramu kukifika tamati Ijumaa, kijana mmoja alitoa ushuhuda ambao uliwaacha waliohudhuria hafla hiyo kulengwa na machozi.
Dennis Mweya alisimulia jinsi unywaji pombe haramu umemwathiri kwa zaidi ya miaka kumi na kupoteza si kazi tu, bali rafiki wake wa Karibu, na hata wakati si mmoja kuponea kifo baada ya kunywa pombe na kupigwa na wakora ambapo nusura kukatwa mguu wake wa kushoto.
Mweya alichukua mda wake kuelezea majanga amepitia kutokana na unywaji pombe haramu, huku akionyesha umati uliobaki vinywa wazi, baadhi ya sehemu muhimu za mwili alizopoteza na kushonwa kutokana na kukatwa na vifaa vyenye makali.
Mwathiriwa huyo, ambaye alifanya kazi ya uhasibu kwenye chuo kikuu cha Kisii amepoteza zaidi ya nusu ya idadi ya meno yake, aliwaacha watu na tabasamu alipodokeza kuwa yupo katika kituo cha urekebishaji wa tabia na ushauri nasaha wa chuo Kikuu cha Kisii, na kuahidi kupambana hadi mwisho ili kuachana kabisa na pombe.
Jamaa huyo wa umri wa miaka 32 aliwasihi vijana, hasa wanafunzi, kuepukana na makundi ya vijana potovu, huku akijutia mwelekeo aliofuata kutoka kwa vijana wenzake akiwa shule ya upili.
“Singependa kuona kijana yeyote kupitia hali ambayo nimepitia, nimehangaika maishani, nawaomba mwachane na pombe na dawa za kulevya mmejionea; sina meno, uso wangu umesurumbuka na kuchanika 'just quit today',” alisihi Mweya.