Gavana wa Kwale Salim Mvurya ameeleza kutofurahishwa kwake na joto la kisiasa linalozidi kushuhudiwa katika kaunti hiyo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Haya yanajiri baada ya Mvurya kujiunga na chama kipya cha Jubilee Party.

Baadhi ya wafuasi na wanasiasa wa ODM wamemtaja kama msaliti kutokana na kujiunga na upande wa serikali.

Akizungumza katika hafla ya kuchangisha fedha za kundi la wazee katika kijiji cha Tawi, Mvurya alisema hawezi kujibu maneno hayo.

Alisema kuwa wapinzani wake katika Kaunti ya Kwale wataendela kuongea lakini raia ndio watakuwa wa jukumu la kusema na kuamua.

"Vyombo vya habari vimekuwa na furaha sana kubeba majibizano ya kila kiongozi lakini mimi siko katika ligi hiyo. Kitu muhimu ni kuhakikisha kuwa watu wangu wamepata huduma nzuri,” alisema Mvurya.

Aidha, aliwahimiza wakaazi wa Kwale kutoathiriwa na joto hilo la kisiasa na badala yake kuishi kwa amani.

"Mimi sitaki kuwaona mkipigana kwa sababu za kisiasa. Kama ni mimi naongelewa, najua vile ntajitetea vizuri. Msipigane kwasababu yangu,” alisema Mvurya.