Aliyekuwa mbunge wa Kitutu Masaba Walter Nyambati amesema hataunga mkono mwanasiasa yeyote katika kaunti hiyo katika wadhifa wa kiti cha ugavana mwaka wa 2017.
Nyambati amesema yeye atakiwania kiti hicho kwani yuko tayari kubadilisha kaunti hiyo kimaendeleo huku akisema kaunti hiyo iko chini zaidi kimaendeleo na anahitaji kuifufua
Kulingana na Nyambati, aliyezungumza mjini Nyamira siku ya Jumatatu, alikanusha madai ya wale ambao wanasema huenda aunge mkono mmoja wa wawaniaji wa kinyanganyiro hicho cha ugavana, na kusema yeye mwenye atakiwania hadi debeni.
“Mimi niliamua kujitoza katika kinyanganyiro cha ugavana hapa Nyamira baada ya kushuhudia maendeleo kutofanywa jinsi inavyostahili, na ninahitaji kufanya mengi,” alisema Nyambati.
Aidha, mbunge huyo wa zamani alisema idadi kubwa ya wakazi wa kaunti hiyo wamekuwa wakimwomba kuwania kiti hicho, jambo ambalo aliitikia na kusema atajaribu kila awezalo kubadilisha na kuleta maendeleo ikiwa atachaguliwa.