Huku kampeni za kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa mwaka wa ujao zikizidi kupamba moto nchini, Seneta wa kaunti ya Mombasa Hassan Omar amesema yuko tayari kupimana nguvu katika ubabe wa kisiasa kwenye kinyang’anyiro cha ugavana wa kaunti ya Mombasa.
Omar amesema kuwa kamwe hatatingishwa na matamshi ya wabunge wa kaunti hiyo wanaodai kuwa ana muhujumu gavana wa kaunti ya Mombasa pamoja na kuikosoa serikali ya kaunti hiyo bila misingi yoyote.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumapili, Omar alisema kuwa kila Mkenya ana haki kikatiba kuwania wadhfa anaouenzi, lakini matamshi ya bunge la kaunti ya Mombasa ya kumtaka asubiri hadi mwaka wa 2022 hayana misingi yoyote.
“Sitatingishwa na matamshi ya bunge la kaunti ya Mombasa wanaodai ati nisubri hadi mwaka wa 2022, Kenya ni nchi ya demokrasia na niko na uhuru wa kuwania kiti ninachokihitaji kutokana na kuwa wananchi wenyewe ndio waliyonipendekeza ili kuwatekelezea mahitaji yao na kubadili uongozi duni wa kaunti ya Mombasa," alisema Omar.
Omar alliongeza kuwa atahakikisha amezuru hadi mashinani kuonana na wakazi wa kaunti hiyo na kuendeleza sera zake kwani yuko na imani kuwa wakazi wa kaunti ya Mombasa watajitokeza kwa wingi na kumchagua, huku akiwarai kuhakikisha kuwa wanajisajili kuwa wapiga kura.
Siasa za kaunti ya Mombasa zimeonekana kubadili mkondo mpya huku viongozi wanaonekana kumezea kiti hicho cha ugavana ni pamoja na Naibu Gavana wa kaunti hiyo Hazel Katana, Mbunge wa Nyali Hezron Awiti, mfanyibiashara wa kaunti ya Mombasa Suleiman Shahabal, Gavana wa kaunti hiyo Ali Hassan Joho.