Mzee Ngala amekanusha madai kuwa ananuia kustaafu muziki na kumwachia mwanawe Jimmy Ngala kuendeleza gurudumu hilo.
Kwenye mahojiano na mwandishi huyu siku ya Alhamisi, Mzee Ngala anayejulikana sana kama mwanzilishi wa muziki wa Bango, alisema kuwa hawezi kustaafu kuimba muziki huo kwa kuwa hakuna binadamu anayeweza kusitisha kipaji ambacho hakijatumika.
Alisema kuwa bado anasiha njema na bado anao uwezo wa kutunga na hata kumwaga sauti kwenye vinasa sauti na hatimaye kuachilia bango safi ikilinganishwa na zile alizotoa hapo awali.
Madai hayo yalijiri siku chache tu baada ya mwanamuziki kutoka Tanzania Mzee Yusuf kutangaza kustaafu muziki, jambo lilowafanya mashabiki kutaka kujua iwapo Ngala pia angechukua hatua hiyo.
“Kipaji changu ni kama baraka kutoka kwa Mola na kila ninapotunga nyimbo kwa waharusi, wengi wa mashabiki hunifata na kuniitisha nyimbo hiyo. Mashabiki wangu ndio hunipa msukumo zaidi wa kuhakikisha kuwa nabaki katika ulingo wa bango ili kuzidi kutoa ngoma zinazowafurahisha,” alisema Ngala.
Aidha, alisema kuwa kipaji chake ndicho kilichomsaidia kuwekeza kwenye biashara mbalimbali anazomiliki na hata kutosheleza mahitaji ya kifamilia pamoja na kuwaelimisha watoto wake.
Alisema sharti akitumie kipaji hicho vilivyo kwa maana sio wengi waliobarikiwa na uwezo wa kuimba, kwa hivyo ni lazima atumie akili na sauti yake kuwatumbuiza.