Wachuuzi katika soko la Marikiti mjini Mombasa wamelalamika vikali kuhusu ukosefu wa huduma za vyoo sokoni humo, jambo ambalo wamesema limeathiri biashara zao vibaya.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumzia swala hilo, Katibu Mkuu wa soko hilo Mahmud Abdalla alidokeza kuwa ukosefu huo umewatia aibu machoni mwa wateja wao ambao hulazimika kutafuta njia mbadala za kutimiza haja zao.

"Tumekuwa na aibu sana kwa wateja wetu ambao inawalazimu kutumia vyoo vya kibinafsi ambavo hutoza ada," alisema Abdalla.

Katibu huyo alisema kuwa ni ishara mbaya sana kwa wateja ambao hulazimika kutumia vyoo vya kulipa, jambo ambalo huwatia wao na wateja hao katika hatari za kiafya. 

Wachuuzi wa soko hilo wametoa wito kwa Serikali ya Kaunti ya Mombasa kushughulikia suala hilo na kuwajengea vyoo ili kuwakinga na mikurupuko ya magonjwa ya uchafu kama kipindupindu.

Hata hivyo, Waziri wa Afya Kaunti ya Mombasa Mohamed Omar amesema wanasoko hao ndio kikwazo kwa sababu hawajaitoa nafasi ya kujengwa vyoo hivyo. 

"Mpaka watoke pahali hapo ndipo tuwajengee vyoo. Kama sivyo basi hatuna namna nyingine," alisema Bw Omar.