Wakaazi wa kaunti ya Kisii wana kila sababu ya kutabasamu, baada ya Gavana wa kaunti James Ongwae kutangaza kuwa soko zote 24 zilizoko katika kaunti hiyo zitawekewa mataa ili wafanyibiashara wawe wakifanya biashara zao masaa 24 kama njia mojawapo ya kuinua uchumi wa kaunti hiyo.
Akizungumza siku ya Jumamosi katika mji wa Kisii, Ongwae alisema mikakati imekamilika ya kuweka mataa hayo kwa soko zote ili wananchi pamoja na wanabiashara wawe wanafanya shughuli zao kila siku kwa masaa 24.
“Kwa miezi miwili ijayo, soko zote zitakuwa zimewekewa mataa ya kumulika, na mimi kama gavana nahitaji kuona uchumi ukiinuka zaidi katika kaunti hii kupitia biashara pamoja na kilimo,” alisema Ongwae.
Wakati huo huo, wakaazi, ambao wengi ni wafanyibiashara walimpongeza gavana kwa mradi huo, kwani wengine wamekuwa wakisumbuka sana haswa giza linapoingia.
“Vile gavana amesema kuwa ataweka mataa kwa soko zetu, mimi kama mwanabiashara nitafurahi sana ili tuwe tunafanya biashara hata usiku na mchana bora tupate riziki ya kila siku,” alihoji Zipporah Ombachi, mwanabiashara wa mboga ali maarufu mama mboga.