Seneta wa Nairobi Mike Sonko amesema atasimamia gharama ya matibabu ya manusura wa shambulizi la kigaidi lilotokea katika kanisa moja wilayani Likoni, mjini Mombasa, miaka miwili iliyopita.
Sonko alisema kuwa atagharamia matibabu ya waathiriwa hao wawili walionusurika na majeraha ya risasi, ambao kwa sasa wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Kijabe.
Akiongea siku ya Jumapili wakati wa ibada maalum ya kuathimisha miaka miwili tangu shambulizi hilo kutokea katika kanisa la Joy in Jesus, Sonko pia aliahidi kusaidia familia zilizoathirika na mkasa huo.
“Nitatumia uwezo nilionao kuhakikisha kuwa nasaidia familia hizi ambazo zinapitia hali ngumu,” alisema Sonko.
Seneta huyo alikuwa ameandamana na Satrine Osinya, mtoto mdogo aliyenusurika wakati wa shambulizi hilo.
Ahadi ya Sonko ya kugharamia matibabu ya manusura hao imetoa matumaini makubwa kwani baadhi ya waathiriwa hao wanaopitia hali ngumu ya maisha huku hata baadhi ya wale waliopona wakibaki na ulemavu.
Shambulizi hilo lilitokea mwezi Machi mwaka 2014 baada ya magaidi wawili kuvamia na kufyatulia waumini risasi. Watu wanne wakiwemo wazazi wa Osinya walifariki huku zaidi ya watu 15 wakijeruhiwa.