Seneta wa Nairobi Mike Sonko ameilaumu afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma kwa kujikokota kuendesha kesi inayoikabili vuguvugu la MRC.
Sonko alisema kuwa kesi hiyo ni ya kitambo na mpaka sasa bado haijulikani kikomo.
Seneta huyo aliiambia Mahakama ya Mombasa siku ya Ijumaa kuwa kesi hiyo imechukua miaka minne kufikia sasa bila kukamilika licha ya wanachama wa vuguvugu hilo kuhudhuria vikao vya kesi hiyo.
“Kesi hii ni ya zamani ilhali bado inasikizwa kwa mwendo wa kobe,” alisema Sonko.
Haya yanajiri baada ya Sonko kutakiwa kuelezea aliko mwenyekiti wa MRC Omar Mwamnuadzi.
Sonko amekuwa mdhamini wa Mwamnuadzi tangu kukabiliwa na mashtaka hayo.
Wakati huo huo, Sonko ameitaka mahakama kumpa muda wa miezi miwili kuweza kumtafuta mwanachama huyo.
“Naomba kupewa miezi miwili kuweza kumtafuta kiongozi wa MRC,” alisema Sonko.
Seneta huyo aliahidi kushirikiana na familia ya kiongozi huyo ili kumfikisha mahakamani.
Ikumbukwe kuwa agizo la kukamatwa kwa Mwamnuadzi lilitolewa miezi miwili iliyopita kwa kususia vikao vya kesi hiyo.
Mwamnuadzi i na wenzake zaidi ya 20 wanakabiliwa na mashtaka ya kuandaa mkutano kinyume cha sheria na kuwa wanachama wa kundi la MRC.
Kesi hiyo itatajwa tena Novemba 23, 2016.