Mahakama ya Mombasa imempa Seneta wa Nairobi Mike Sonko siku 90 kumtafuta kiongozi wa vuguvugu la MRC, Omar Mwamnuadzi.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Hakimu Dauglous Ogoti amesema iwapo Sonko atashindwa kumtafuta Mwamnuadzi, basi hatua itachukuliwa dhidi yake, ikiwemo kumpokonya shamba lililotumika kama udhamini dhidi ya Mwamnuadzi.

Haya yanajiri baada ya Sonko kuiambia mahakama kuwa kufikia sasa ameshindwa kumpata Mwamnuadzi, na kuomba kupewa muda zaidi wa siku 90 ili kuweza kushirikiana na polisi kumsaka.

“Ninatoa muda wa miezi mitatu kwa Sonko kumsaka kiongozi wa vuguvugu la MRC Omar Mwamnuadzi, la sivyo shamba lake lichukuliwe na serikali,” alisema Ogoti.

Sonko, kupitia wakili wake Jerad Magolo, amesema kuwa kuna fununu kwamba Mwamnuadzi alienda mafichoni nchini Tanzania.

“Kuna tetesi kuwa Mwamnuadzi alienda mafichoni Tanzania,” alisema Magolo.

Mwamnuadzi na wenzake zaidi ya 20 wanakabiliwa na mashtaka ya kuandaa mkutano kinyume cha sheria na kuwa wanachama wa kundi la MRC.

Sonko amekuwa mdhamini wa Mwamnuadzi tangu kukabiliwa na mashtaka hayo.

Kesi hiyo itatajwa tena March 7, mwaka ujao.