Seneta wa Nairiobi Mike Sonko amesema yuko tayari kuelekea nchini Marekani kujitetea kwa tuhuma za ulanguzi wa dawa za kulevya.
Kauli yake inajiri baada ya kitengo cha kukabiliana na dawa za kulevya kutoka Marekani kuanza kuchunguza upya faili za wanasiasa wanaodaiwa kuhusika katika ulanguzi wa dawa za kulevya.
“Niko tayari kuenda kujitetea kuhusiana na swala hilo,” alisema Sonko.
Akizungumza katika eneo la Changamwe siku ya Jumapili, Sonko aliwataka washukiwa wote wa biashara hiyo haramu kuwa tayari kukabilana na mkono wa sheria badala ya kueneza porojo katika vyombo vya habari.
Miongoni mwa waliotajwa katika ripoti hiyo miaka sita iliyopita ni Seneta wa Nairobi Mike Sonko, Gavana wa Mombasa Hassan Joho, Waaziri wa kitambo Haron Mwau, Mbunge wa Kamukunji Simon Mbugua, Mbunge wa Othaya Mary Wambui na Gavana wa Kiambu William Kabogo.
Haya yanajiri baada ya wana wa marehemu Akasha na raia wawili wa kigeni kupelekwa Marekani kufunguliwa mashtaka ya ulanguzi wa mihadarati.