Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Walimu waastaafu chini ya kundi la mwaka wa 1997 wapatao 52,000 wamemtaka katibu mkuu wa muungano wa waalimu kitaifa wa KNUT Wilson Sossion kujiepusha kabisa na maswala yanayowahusu.

Hayo yanajiri baada ya Sossion kunukuliwa Jumatano kwenye jarida moja la hapa nchini akisema kwamba amempa mkurugenzi wa malipo ya uzeeni pamoja na tume ya kuajiri walimu nchini TSC siku 30, kulipa waalimu hao wastaafu shilingi bilioni 42.3 kama ilivyoagiza mahakama.

Wakiongea na wanahabari Alhamisi mjini Nakuru, viongozi hao wakiongozwa na mwenyekiti David Mwenja na katibu Gidraph Kimatta, walisema kwamba sasa wao sio wanachama wa KNUT na kwa hivyo Sossion hana mamlaka yoyote ya kutolea serikali makataa kuwahusu.

“Kwa Sossion kujidai kwamba anatetea waalimu wastaafu kwa kutolea serikali makataa ya siku 30, anadhihirisha msimamo wa kupotosha, kinyume cha katiba ya KNUT na usio na nia njema” alisema Mwenja.

Aidha alisema kwamba hakuna wakati hata mmoja Sossion, kama katibu wa KNUT, aliwahi kufika mahakamani wakati ambapo walimu wastaafu waliwasilisha kesi mahakamani, na iliyodumu kwa miaka 10.

Hata hivyo Kimatta alimtaka Sossion kuomba kiti chochote cha kisiasa kama ana nia hiyo, lakini kukoma kujificha nyuma ya walimu wastaafu ili kujipatia umaarufu.