Katibu mkuu wa muungano wa walimu nchini KNUT Wilson Sossion amepinga vikali kuondolewa kwa mfumo wa elimu ya 8-4-4 akidai kuwa kunahitajika mazungumzo zaidi kabla ya kubatilisha mfumo huo.
Sossion ambaye alikuwa akizungumza katika kanisa la PCEA la Bishop Arthur jijini Nakuru siku ya Jumapili, alielezea kuwa tatizo la elimu nchini ni uhaba wa walimu na malipo duni kwa walimu nchini ila si mfumo.
"Kama walimu tumesimama kidete kupinga hatua ya kubadilisha mfumo wa elimu nchini iwapo maslahi ya walimu hayataangaziwa kwanza. Shida zinazokumba sekta ya elimu zitaendelea kushuhudiwa hata mfumo utakapobadilishwa iwapo shida zetu hazitasuluhishwa," Sossion alisema.
"Serikali inafaa kuajiri walimu zaidi na kuboresha malipo yao ili kuimarisha viwango vya elimu nchini," Sossion aliongezea.
Katibu huyo mkuu wa KNUT pia ameomba wadau katika sekta ya elimu kuwa na subira ili wasije wakajutia baadaye na mfumo huo mpya. Haya yanajiri baada ya rais mstaafu Daniel Moi kukataa mfumo mpya wa 2-6-6-3 ambao umependekezwa na wadau katika sekta hiyo.