Katibu Mkuu wa Chama cha Waalimu nchini (KNUT) Wilson sossion ameomba Rais Uhuru Kenyatta kuwatia mbaroni wale waliotajwa kuhusika moja kwa moja na kundi haramu la Al-Shabab aidha kwa ufadhili au kwa ushirika wowote ule ili kukandamiza jinamizi hili la uhalifu nchini.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

 

Sossion alisema haya aliposhiriki mkutano mkuu wa elimu Wilayani Borabu siku ya Alhamisi ambapo pia alimtaka Rais Uhuru kuwazurutisha viongozi wa kisiasa kutoka Kaskazini Mashariki kuwatambua waahalifu na wanachama wa Al-Shabaab walivyodai.

“Wakenya hawawezi kuwekwa mateka kwa muda wa mwezi mmoja na viongozi kutoka Kaskazini Mashariki eti wameitisha muda wa mwezi mmoja kuwasema wanachama wa Al-Shabaab huku mauaji yakiendelea kote nchini,” alisema Sossion.

Katibu huyo pia aliwataka walimu wote watoke katika eneo hilo kwa minajili ya usalama wao huku akiitaka Serikali kutowaadhibu walimu hao wanapokimbilia usalama wao sehemu zingine nchini.

“Hamna haja kwa shirika la kuwaajiri walimu kuwafuta kazi walimu ambao wameonyesha nia ya kutoa huduma zao kwingineko kando na eneo la Kaskazini Mashariki,” alisema Sossion.

Alihoji pia kuwa Vyuo vyote na Taasisi zilizoko katika eneo hilo zifungwe na huduma zao kuelekezwa mahala kwingine kulioko na usalama wa kutosha akisisitiza kuwa Chuo Kikuu cha Garissa kufungwe kabisa maoni yake yakiwa kigeuzwe na kuwa kituo cha kutoa mafunzo kwa wanajeshi.

Kuhusu kufunga kwa kambi ya wakimbizi, Sossion alidai kuwa ni jambo la busara kufunga hasa kambi ya wakimbizi ya Kakuma walakin akawataka viongozi kutoka eneo la Kaskazini Mashariki kuwajibikia wakenya kwa kuwaweka wazi wahalifu.

Kulingana na Sossion, kufungwa kwa matawi ya ubadilishaji hela, kutuma na kupokea almaarufu ‘Hawala’ kutafanikiwa ikiwa pia viongozi wengine Serikalini wanaounga mkono magaidi hao watawekwa wazi kwa kuwa ilivyo ni kwamba magaidi wana uungwaji mkono kutoka sehemu nyingi.

Aidha alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kutolegeza kamba katika vita vyake dhidi ya ufisadi akiongeza kuwa ufisadi limekuwa donda sugu lenye linapaka tope kila Serikali ilioko mamlakani.