Spika wa bunge la kaunti ya Kisii Okerosi Ondieki ameagiza kiongozi wa walio wengi katika bunge hilo Protus Moindi kufikisha ripoti katika bunge hilo ili kueleza miradi ambayo imefanywa na serikali ya kaunti hiyo katika mwaka 2015/2016 na ni miradi ipi ya maendeleo ambayo ingali inaendelea.
Agizo hilo lilitolewa na spika baada ya baadhi ya wawakilishi wa wadi katika bunge hilo wakiongozwa na Mwakilishi wa wadi ya Magenche Timothy Ogugu kuomba kuona ripoti hiyo ili kujua ni miradi ipi imefanywa na ni ipi inaendelea.
Akizungumza siku ya Jumatano katika bunge hilo spika wa bunge hilo Okerosi Ondieki alisema ni haki kwa kila Mwakilishi kujua yale yamefanywa na yenye yanaendelea kufanywa ili kueleza wakaazi wa wadi yake.
“Ni haki kwa kila Mwakilishi kujua maendeleo ambayo yamefanywa kwa wadi yake na ni miradi ipi inaendelea kufanywa ili kuonyesha uwazi katika maendeleo ya kaunti ya Kisii,” alisema Ondieki.
“Naomba kiongozi wa walio wengi kuleta ripoti hiyo ifikapo juma lijalo siku ya jumanne katika bunge hili letu,” aliongezea Ondieki.