Spika wa bunge la Seneti Ekwe Ethuro amewakosoa magavana kwa kuendeleza ufisadi mashinani na kushindwa kusimamia vyema fedha za umma.
Ethuro amesema kuwa magavana wengi wameshindwa kueleza ni vipi wametumia fedha hizo huku wengi wao wakizitumia kwa maslahi yao ya kibinafsi badala ya kuboresha huduma za wakaazi.
Akizungumza katika hafla ya kufuzu kwa wanafunzi wa masomo ya utabibu katika chuo cha utabibu cha North Coast huko Kikambala, Ethuro amesema kuwa magavana wengi wameongeza kodi kwa asilimia kubwa kwa wafanyibiashara mashinani hali inayowakandamiza.
“Magavana wameshindwa kueleza vipi wametumia fedha za umma kutokana na utumizi mbaya na hatua hiyo ni mbaya kwani wanawakandamiza wakenya wanaotoa ushuru bila ya kufanyia maendeleo,” alisema Ethuro siku ya Jumamosi.
Kauli ya Ethuro imeungwa mkono kikamilifu na seneta wa Kaunti ya Mombasa Omar Hassan Sarai aliyesisitiza kuwa lazima Magavana wawajibikie kikamilifu kuhakikisha kuwa fedha zinazosambazwa mashinani zinatumika vyema.
Sarai amewashinikiza wakaazi wa kaunti ya Mombasa kutoa sauti yao kuhusiana na uadilifu miongoni mwa viongozi na akahoji kuwa iwapo Gavana atashindwa kuyatekeleza majukumu yake kikatiba anafaa kuondolewa mamlakani.