Spika wa bunge la kaunti ya Nyamira Joash Nyamoko amejitokeza kuwaomba wawakilishi wadi katika kaunti hiyo kufanya kazi kwa pamoja bila ya kuzingatia vyama vya kisiasa wanavyoegemea.
Kwenye kikao na wanahabari katika mkahawa mmoja mjini Nyamira siku ya Jumanne, Nyamoko alisema kwamba wawakilishi wadi katika bunge la kaunti ya Nyamira wafaa kushirikiana ili kuwafanyia wananchi kazi.
"Ninawahimiza wawakilishi wadi katika kaunti hii kushirikiana ili kuhakikisha kwamba wanafanya kazi kwa pamoja hasa kwa kuunga mkono miswada yenye manufaa kwa wananchi bila ya kuzingatia vyama wanavyoegemea," alisema Nyamoko.
Nyamoko aidha aliongeza kuwahimiza wanachama wa kamati mbalimbali katika bunge la kaunti hiyo kupunguza muda wanaotumia kufanya vikao ili kuandika ripoti zao.
"Najua kwamba wanachama wa kamati mbalimbali bungeni wanafanya kazi nzuri, ila ningependa kuwahimiza kutumia muda mchache kwenye vikao ili kumaliza kuandika ripoti zao kwa maana hali hiyo itasaidia kuokoa pesa zinazotumika kwenye vikao hivyo," aliongezea Nyamoko.