Kufuatia Bunge la Kaunti ya Kisii kuvunjilia mbali Kamati ya Bunge ya Kaunti ya Huduma kwa Umma (County Assembly Service Board), sasa Wawakilishi hao wamesema watamchunguza Spika wa Kaunti hiyo Kerosi Ondieki ambaye aliongoza Kamati hiyo.
Kamati hiyo ambayo imekuwa ikilimbikiziwa shutuma za kupitisha kiwango kikubwa cha zaidi ya Sh9 milioni cha bima kwa Wawakilishi wa Wadi ambacho kilitiliwa shaka na kuzua mtafaruku mkubwa miongoni mwa Maafisa wa Kaunti hiyo ambapo ilibidi uchunguzi uanzishwe na Bunge hilo.
Kufuatia hatua hiyo ya kubatilishwa kwa Kamati hiyo siku ya Jumatano jioni, Bunge la Kaunti limemteua Mwakilishi wa Wadi ya Bochi Borabu Samuel Onuko kusimamia Kamati teule ya muda kwa kipindi cha siku saba huku wakijiandaa kuteua kamati ya kudumu baadaye.
Kashfa hiyo ambayo ililihusisha Bunge hilo kilizua malumbano makubwa baina ya Spika na Kamati angalizi ya Kaunti hiyo ya Kisii mapema mwezi Aprili ambapo baadhi ya wafanyibiashara katika mjini huo walitishia kuwapeleka Kortini wahusika kama Bunge hilo lingefeli kuwajibika.
Hata hivyo hii ni hatua mojawapo ya Kaunti ya Kisii kutia juhudi za kuonyesha kuwa wanapigana na ufisadi kufuatia wakaazi wengi kulalama kuwa Kaunti hiyo imekuwa ikipendelea watu Fulani kupata kandarasi za Kaunti na wale wanafuzu kupewa ‘Kadi nyekundu’.