Mkurungenzi mkuu wa shirika la utetezi wa haki za kibinadamu la Haki Afrika nchini Hussein Khalid amesema kuwa kila mwananchi ana haki kikatiba kuhakikishwa usalama dhabiti katika maeneo yake.
Kwenye mkao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Khalid alisema kuwa kipengele cha 29 katika katiba ya nchi inaangazia vyema jinsi serikali inavyostahili kumpa usalama mwananchi huku akisema kuwa jukumu hilo linstahili kutekelezwa zaidi na idara ya usalama nchini.
Khalid amesema kuwa licha ya kuwa na changamoto za kiusalama nchini na hususan eneo la Pwani ipo haja ya serikali, wadau mbalimbali katika maswala ya kiusalama na mashirika ya kijamii kujitokeza na kuhakikisha kuwa mwananchi analindwa vyema.
Aidha anasema kuwa kufuatia dhulma za kihistoria katika maeneo ya pwani, suala la usalama limeonekana kusaulika na akasisitiza kuwa swala hilo linapaswa kupewa kipau mbele ili eneo hili kuwa salama na kuzuia visa vya unyanyasaji.
"Tungependa kuishnikiza serikali kuhakikisha kuwa inazingatia katiba ya nchi hasa swala la usalama kupewa kipau mbele na kuwalinda wananchi dihdi ya uhalifu ili taifa hilo na hususan eneo la pwani kuwa salama," alisema Khalid.
Kauli ya Mwaharakati huyo imejiri baada ya kaunti ya Mombasa na Lamu kushuhudia maafisa wa polisi wakiwatia nguvuni washukiwa wa ugaidi huku wengine wakijeruhiwa na kutoroka.