Afisaa mkuu mtendaji wa bodi ya huduma za maji eneo la bonde la ufa mhandisi Japheth Mutai amewahakikishia wakaazi wa eneo hili kwamba tatizo la kubadili rangi ya meno na mifupa hafifu litapata suluhu hivi karibuni.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza na wanahabari afisisni mwake Ijumaa hii mjini Nakuru, Mutai alisema kuwa viwango vya madini ya flouride kwenye maji katika eneo hio, la kati ya miligramu 4 hadi 8 kwa kila lita ya maji, imezidi kiwango kinacho pendekezwa na shirika la afya ulimwenguni (WHO) cha chini cha miligramu 1.5 kwa lita ya maji.

Mutai alisema kuwa suluhu hiyo inatokana na mpango wa ujenzi wa bwawa la maji la Itare hivi karibuni ,linalonuiwa kukamilishwa baada ya muda wa miaka mitatu ijayo.

Kwa mujibu wa kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya maji ulimwenguni iliyofanyika mwezi machi ambayo ni maji na ajira, mhandisi huyo anashilikia kuwa ukosefu wa nafasi za ajira kwa vijana wengi, hususani katika vikosi vya jeshi kutokana na kubadili rangi ya meno kutoka nyeupe hadi hudhurungi au brown itazikwa katika kaburi la sahau.

Ingawa bodi hiyo inasimamia miundo msingi ya maji katika kaunti saba ikiwemo Nakuru, Narok, West Pokot, Elgeyo Marakwet, Baringo, Nyandarua, Turkana ambayo inahudumia zaidi ya watu milioni sita, Mutai ametaka maji yanayopatikana kwa sasa kutumiwa vyema.

Vile vile ameshikilia kwamba upungufu wa maji unaoshuhudiwa kwa sasa utamaliza katika siku za hivi karibuni.

Matamshi hayo yanajiri baada ya rais Uhuru Kenyatta kuahidi mnamo mwezi machi mwaka huu, kuzindua mradi wa ujenzi wa bwawa la maji la itare kabla ya mwisho wa mwezi wa sita mwaka huu utakaogarimu serikali shilingi bilioni 38.