Huku mgogoro kuhusiana na kubanduliwa kwa Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC ukichacha, Baraza kuu la SUPKEM limekosoa mbinu zinazotumiwa na mrengo wa CORD kuiondoa tume hiyo mamlakani.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mwenyekiti wa baraza hilo, Profesa Abdulghafur El-Busaidy, amesema kwamba mgogoro huo utatatiza mshikamano wa taifa.

Akizungumza siku ya Ijumaa mjini Mombasa, El-Busaidy alisema kuwa ipo haja ya viongozi kuafikiana kuhusu jinsi ya kutatua suala hilo.

El-Busaidy alisema kwamba maswala kama hayo ya kitaifa yanapaswa kutatuliwa kwa kuzingatia uiano wala sio mabishano na maandamano ambayo tayari yamezua taharuki nchini.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo wa SUPKEM aliitaka IEBC kuwafafanulia Wakenya majukumu yake na kuweka wazi utaratibu wake wa kuandaa uchaguzi mkuu ujao ili kuregesha imani ya Wakenya.

“Tunaitaka Cord kutumia njia za kisheria kushinikiza kubanduliwa kwa IEBC. Tume hiyo pia inapaswa kuweka wazi utendakazi wake ili Wakenya wawe na imani nayo,” alisema El-Busaidy.

Kauli ya baraza hilo kuu la Waislamu nchini inajiri huku mirengo ya CORD na Jubilee ikivutana kuhusiana na kubanduliwa mamlakani kwa makamishna wa Tume ya IEBC, huku CORD ikitaka majadiliano na serikali.