Susumila, msanii tajika kutoka Mombasa, amesema atashirikiana na wasanii chipukizi kuhakikisha sanaa ya uimbaji kanda ya Pwani inakua na kutambulika kote Afrika Mashariki.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Susumila, ambaye kwa sasa anaendelea kufanya vyema kwenye ulingo wa burudani hasa kwa kibao chake kipya alichomshirikisha kidosho kutoka kule Nairobi Avril, amesema wakati mwingi wasanii wanaochipuka huwa na talanta lakini wanachokosa ni usaidizi na uelekezi mwema katika ulingo wa burudani.

Akizungumza kwenye mahojiano na kituo kimoja cha radio, Susumila alisema kuwa hatua hiyo husababisha wasanii wengi kuishia kupotea.

“Eneo la Pwani lina wasanii wengi wenye uwezo wa kutunga mashairi yakukubalika ila wanakosa mtaji wa kutosha ili kuanza kuimba. Wengi wao huishia kudhulumika na kukosa watayarishaji wazuri,” alisema Susumila.

Aidha, alisema kuwa watayarishaji wengi huwatumia wasanii hao chipukizi kwa kuiba mistari yao ambayo huwa imesheheni wingi wa ujuzi.

Alisema ni jambo la kusikitisha kuona wasanii chipukizi wakidharauliwa na wenzao wanaotambulika, ilihali pia wao walipitia njia ile ile.

Susu alisema kuwa hangetaka msanii mwengine kupitia mambo aliyopitia, bali anataka wasanii chipukizi waweze kutambulika kwenye ulingo wa sanaa.

Alisema kuwa itambidi kusimama kama promota ili kuwatambulisha wasanii chipukizi kwa mashabiki kwa njia ya haraka.