Susumila, mwanamuziki mashuhuri kutoka Mombasa, amezungumzia uhusiano wake na mwanamuziki mwenza, Escobar.
Haya yanajiri baada ya Escobar kumshirikisha aliyekuwa mke wa Susumila kwenye video ya ngoma Rihoho, inayoendelea kutamba Mombasa.
Susumila amesema kwamba anajua kuwa hiyo ni mambo ya burudani na katu hajachukulia kama kutafutwa kimaneno na Escobar, ambaye ndiye mtunzi na mwimbaji wa ngoma hiyo.
Wanaoenzi muziki hapa Pwani wamekuwa wakisema huenda kukawa na uhasama baina ya wawili hao, kwani Esco amekuwa kimya kwa muda mrefu katika ulingo wa sanaa, ila alipochipuka tena aliamua kuzuka na mwanadada Ruth Rock Immison, na kutoa naye video hiyo.
Susumila amesema kwa sasa hahitaji hata kusikia uvumi wala chochote kuhusiana na swala la 'beef', kwani ana mambo mengi ya kufanya ikilinganishwa na kuanza kutoelewana na msanii mwenzaka.
Aliiongeza kuwa uvumi unaoenezwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na video hiyo zitabaki kuwa tetesi kwani hawezi kurudi katika maisha ya awali.
Alisema kuwa tayari waliachana na mwanadada huyo na kwa sasa ameoa na inampasa kuanza kutekeleza majukumu kama bwana wa mtu na wala sio kuongea ubaya wa wasanii.
Escobar kwa upande wake alisema kuwa hakutarajia namna mashabikii wake walivyochukulia video hiyo kwani wengi wao wamesema kuwa alikuwa akitafuta mzozo baina yake na Susumila.
Alisema kuwa hakutarajia mfarakano kutokea kwani alimshirikisha Ruth kujaliza nafasi ya msichana aliyekuwa anahitajika katika video hiyo.
Hata hivyo amewataka mashabiki wake kujua kuwa hana nia yoyote mbaya na kidosho huyo kwani yeye pia ana familia yake ambayo inamtegemea.