Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mjadala mkali kuhusu umiliki na uendeshaji wa tuktuk mjini Mombasa unatarajiwa kuibuka tena bungeni baada ya bunge la kaunti hiyo kudhibitisha kuwa bado swala hilo halijapata suluhu ya kudumu.

Hapo awali idara ya uchukuzi ilipendekeza kuwa tuktuk zisikubaliwe kuhudumu katikati mwa jiji, agizo lililozua mjadala mkali huku bunge hilo likipinga vikali.

Swala lingine tata linalojitokeza ni agizo kutoka kwa wizara ya uchukuzi kaunti hiyo la kuzuia kusajiliwa kwa tuktuk zingine mpya mjini humo kwa madai kwamba zinasababisha msongamano mkubwa katika barabara za mji.

Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumanne, mwakilishi wa wengi katika bunge la kaunti hiyo Abdallah Kasagamba alisema kuwa wameaanda kikao na wahudumu wa tuktuk ili kutafuta suluhu.

“Kama viongozi wa kaunti tumekaa na wahudumu hao ili kutafuta njia mwafaka kwa sababu ni kweli tuktuk zinaleta msongamano mkubwa barabarani lakini pia kwa upande mwingine lazima tujali maslahi yao kwani wao pia wana haki ya kufanya kazi,” alisema Abdallah.

Mbunge huyo aidha alikiri kwamba msongamano mkubwa wa magari unaoshuhudiwa kila siku mjini humo unasababishwa na tuktuk hizo huku akiongeza kwamba baadhi ya madereva hawafuati sheria za trafiki.

Wakati huo huo kiongozi huyo pia ametoa wito kwa wamiliki wa tuktuk kuwa makini wanapowaajiri madereva akiwasihi kuchunguza na kuhakikisha kuwa ni madereva waaminifu na wenye nidhamu ili kuzuia visa vya uhalifu vinavyohusishwa na tuktuk.

“Tumeweka mikakati ya kughakikisha tunadhibiti tuktuk zote, endapo tuktuk yoyote itahusika katika uhalifu itakuwa rahisi kwetu kufuatilia na kuwanasa wahusika,” aliongeza kiongozi huyo.