Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya ardhi nchini Daktari Mohammed Swazuri ameunga mkono azimio la serikali ya Kaunti ya Mombasa la kuiboresha zaidi Kaunti hiyo kimiundo msingi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ruwaza ya mwaka wa 2035 ya Kaunti ya Mombasa katika uwanja ‘Mombasa Golf Club’ siku ya Jumamosi, Swazuri alisema kuwa miradi hiyo ni mwafaka kwa msingi wa maendeleo ya kaunti.
Kulingana na Swazuri, japo swala la ardhi lingali tata eneo la Pwani, ni vyema iwapo kaunti zitawezeshwa kupata ardhi za kutosha ili kuwekeza katika miradi yake huku akiwakosoa wakazi waliyo na tabia ya kukimbilia mahakamani ili kuipinga miradi hiyo.
Aliwataka wakazi wa kaunti za Pwani kushirikiana na viongozi wao mara kwa mara ili kusukuma mbele kaunti zao kimaendeleo, huku akisema kuwa vita vya kisiasa na migawanyiko vimezirudisha nyuma kaunti za Pwani kimaendeleo.
“Tafadhali wakazi wa Mombasa wacheni tabia ya kwenda mahakamani kupinga miradi inayolenga kuboresha kaunti katika maswala ya kiuchumi na maendeleo na muungane mboresha kaunti ya Mombaa,” alisema Swazuri.
Ruwaza hiyo ya mwaka wa 2035 inalenga kuboresha Kaunti ya Mombasa Kimiundo msingi, mazingira, kitalii, nyumba za makazi miongoni mwa maswala mengine ya kiuchumi, kibiashara na kimaendeleo katika Kaunti hiyo.