Mwenyekiti wa Tume ya ardhi nchini NLC, Mohamed Swazuri, ametoa onyo kwa watu binafsi walionyakua ardhi za shule za umma.
Swazuri amesema kuwa watu hao watakumbana na mkono wa sheria katika siku za hivi karibuni iwapo watadinda kurejesha ardhi hizo kwa shule husika.
Akizungumza katika kongamano la walimu wakuu wa shule za msingi mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Swazuri aliwahakikishia walimu kuwa suala la unyakuzi wa ardhi za shule litatatuliwa na serikali.
“Tutatumia usaroveya kubaini ardhi zote za shule za umma na yeyote atakayepatikana kumiliki ardhi ya shule kwa njia ya unyakuzi atashtakiwa,” alionya Swazuri.
Swazuri aidha amewahimiza walimu wakuu kuwasilisha ombi la kupata hati miliki za ardhi ya shule zao kama njia moja ya kukabiliana na changamoto hiyo.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa tayari tume ya NLC imepokea malalamishi 158 kutoka kwa shule ambazo zinadai ardhi zao zimenyakuliwa na watu binafsi.
Mapema mwaka huu, serikali kuu ilitaka walimu wakuu na bodi za usimamizi wa shule nchini kuanzisha mchakato wa kuchukua hati miliki za shule hizo.