Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi nchini NLC, Mohamed Swazuri, amewataka wakaazi wa Pwani kushirikiana na makamishna na maafisa wa tume hiyo katika juhudi za kukabiliana na unyakuzi wa ardhi katika eneo hilo.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Swazuri alisema kuwa ushirikiano wa dhati pekee ndio suluhisho.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumapili, Swazuri alisema kuwa kesi za unyakuzi wa ardhi katika eneo la Pwani ni nyingi mno na iwapo wenyeji hawatatoka wazi wazi na kulizingumzia swala hilo katika vikao vinavyaandaliwa kila uchao, basi itakuwa vigumu kwa tume hiyo kusitisha unyakuzi wa ardhi Pwani.

Swazuri alisema kuwa atahakikisha kuwa ardhi na raslimali za Wapwani zilizonyakuliwa zimerejeshwa kwa wenyeji, na mabwenyenye waliyonyakua ardhi hizo kuchukuliwa hatua za kisheria.

Aidha, alisema kuwa ni jukumu la tume hiyo kuhakikisha kuwa maswala ya unyakuzi wa ardhi na dhulma za mashamba zinatatuliwa kwa wakati ufaao, ili kusitisha migogoro ya mara kwa mara na kufurushwa kwa wenyeji kwenye ardhi zao na mabwenyenye.

“Sisi tuko tayari kushirikiana na wenyeji kufahamu mengi kuhusu ardhi zilizonyakuliwa ili tuhakikishe kuwa mizozo ya ardhi Pwani inasitishwa. Tutahakikisha wenyeji wanapata haki kulingana na utaratibu tutakaoufuta kutatua shida hiyo,” alisema Swazuri.

Baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na mizozo ya ardhi ni kama vile Mwakirunge, Msambweni, Vipingo, Mariakani, Jomvu, Changmwe, Rabai na maeneo mengine ya Pwani.