Tume ya kitaifa ya ardhi imepuuzilia mbali ripoti iliyochapishwa kwenye mojawapo ya magazeti humu nchini kuwa tume hiyo imeagizwa iondoke kwenye afisi zao zilizo kwenye Jumbe la ardhi jijini Nairobi.
Mwenyekiti wa tume hiyo Mohammed Swazuri akizungumza mjini Nakuru siku ya Ijumaa alisema tume hiyo bado haijapokea stakabadhi yoyote kuonyesha kuwa tume hiyo imeagizwa kuhama.
Swazuri alisema kuwa alifahamu kuhusiana na habari hiyo kupitia kwa taarifa moja iliyochapishwa kwenye gazeti moja la humu nchini.
“Hatujapokea agizo hilo. Hiyo ni fununu tu. Watu hawataki tutekeleze wajibu wetu. Iwapo notisi hiyo ipo, tutaishughulikia wakati huo,' alisema Swazuri.
Mwenyekiti huyo aidha alisisitiza kwamba tume hiyo itasalia katika jumba hilo la ardhi akisema wanaoeneza fununu hizo wanafaa kutafuta majukumu mengine ya kutekeleza.
Pamoja na hayo, alisema shinikizo ambazo zimekuwa zikitolewa katika siku za hivi majuzi hazitapelekea tume hiyo kutofanya kazi yake.
Kuhusiana na kashfa inayozingira swala la ardhi iliyotengewa ujenzi wa barabara ya Eastern by pass, Swazuri alisema kwamba kupitia kwa uchunguzi wa stakabadhi za hapo awali, imebainika kuwa anayetoa mipango ya ujenzi alitoa michoro yake ili kuonyesha kwamba barabara hiyo haiwezi kupitia hapo.
“Kama kawaida tunapoona kipande cha ardhi kisichotumiwa, Wakenya huwa na tamaa ya kutumia kipande hicho. Kipande hicho kimekuwa hakitumiki kwa miaka mingi hadi mwaka wa 1990 au 2000. Mmoja wa wanaotoa mipango ya ujenzi alibadili mpaka wa ardhi hiyo na kuisoongeza kwa mita kadhaa na kisha akachora ramani nyingine ya eneo hilo,” alisema Swazuri.
Alisema kipande hicho cha ardhi kinamilikiwa na serikali kwa sasa na kuwa mamlaka ya barabara za mjini ya KURA inafaa kushauriana na walichonunua kipande hicho cha ardhi ili waweze kufidiwa au hatua mwafaka zichukuliwe.